Na Prof. Umar Ashqar, Mhadhiri Chuo Kikuu cha Jordan
Wakati mwingine, Jini hasa Shetani hawajii watu kwa njia ya kuinong’oneza nafsi ya mtu, badala yake hujitokeza kwao kwa umbile la kibinadamu; au anaweza kusikika sauti yake lakini mwenyewe asionekane. Kwa mfano, kama wewe unaitwa ‘Abdallah’, unaweza ukapita sehemu na kusikia unaitwa, ‘Abdallah!’ lakini ukigeuka huku na huku, huoni mtu, na huoni hata dalili ya kuwepo mtu.
Au Jini anaweza kujitokeza kwa umbile la ajabu-ajabu. Mara nyingi, imesikika kuwa vitu vya ajabu na visivyotambulika vimeonekana vikiruka. Ama vimeonekana vikiruka angani au vimekaa kwa muda fulani ardhini. Watu wengine nao wamesimulia kukutana na viumbe vinavyotofautiana na binadamu, vingine vikiwa kwenye vyombo vya usafiri, ambapo wengine wamedai kuwa viumbe hivyo vimewataka wapande vyombo hivyo.
Madai ya aina hii hayajatoka kwa watu wasiofahamika bali hata watu mashuhuri duniani nao wamesimulia mikasa hiyo. Kwa mfano, Rais wa zamani wa Marekani, mzee Jimmy Carter alisema kuwa aliona viumbe visivyotambulika kule Georgia mwaka 1973.
Akaanzisha utafiti juu ya kuwepo kwa viumbe vingine ambavyo vimevamia duniani. Aliweza kuzungumza jambo hilo na mwanasayansi mmoja aliyeamini kuwa vipo viumbe vingine. Pamoja na Jimmy Carter, alikuwepo pia mshauri wake wa Masuala ya Sayansi, Frank Price.
Baadae Jimmy Carter akaangalia filamu moja iliyoelezea tafiti zilizofanyika kuhusiana na kuwepo kwa viumbe vingine vinavyoishi anga za juu. Mtu aliyeonesha filamu hiyo alikuwa ni Mkuu wa Idara ya Astronomia katika Chuo Kikuu cha Cornell, Bw. Carl Sagan. Huyu ndiye mtaalamu ambaye Mamlaka ya Anga ilikuwa ikimtegemea kujibu swali la kuwepo kwa viumbe vingine katika sayari nyingine. (Taz. Jarida la al-Siyasa al-Kuwaitiya, Na. 3399, Mei 12, 1977).
Aidha iliripotiwa katika Jarida moja la Kuwait kwamba Rais wa zamani wa China, hayati Mao Tse Tung naye aliamini kuwepo kwa viumbe vinavyoishi katika sayari nyingine. Mwandishi wa ripoti ya Jarida hilo alibainisha kuwa asilimia 61 ya Vijana wa Amerika wanaamini kuwa vipo viumbe visivyotambulika. Na kwa mujibu wa magazeti ya Marekani, takribani nusu milioni ya Wamarekani wameviona viumbe hivyo ambavyo wenyewe wanaviita “Unidentified Fying Objects-(UFOs).”
Miaka michache baadae mcheza filamu Steven Spielburg alitengeneza senema iliyoitwa Close Encounters of the Third Kind, ambayo iligharimu dola za Marekani milioni 22. Filamu hii ilichezwa baada ya kukusanya taarifa zote zilizohusu kuonekana au kukutana na viumbe visivyotambulika. Filamu hiyo kwanza ilioneshwa ndani ya Ikulu ya Marekani ambapo mtu wa kwanza kuiona alikuwa ni Rais.
Baada ya hapo filamu ikasambaa, Mamlaka ya Anga ikaridhika kuwa ni jambo muhimu kufanya utafiti wa suala hilo. Mnamo mwaka 1979, zikatengwa dola milioni moja kwa ajili ya utafiti huo. Walianza na mradi wa siri ulioitwa SITY na wakatega vifaa maalum kubaini kama hao walikuwa ni viumbe waliovamia dunia kutoka sayari nyingine.
Hapa tufichue nukta zifuatazo:
(i) hakuna hoja ya kukanusha kuwepo kwa viumbe wengine wa ajabu ambao ni tofauti na binadamu. Taarifa za kuonekana kwa viumbe hao zimeendelea kuwepo kwa kipindi cha karne ishirini zilizopita, kwa kweli, ni kwa zaidi ya karne mia. Mimi (Profesa Ashqar) nilifanya utafiti wa jambo hili kwa kipindi fulani, na nikagundua makala moja iliyozungumzia jambo hilo kila wiki au zaidi.
Tukio la hivi karibuni kabisa lilitokea nchini Kuwait ambako zaidi ya mtu mmoja wameripotiwa kusema kuwa wameona viumbe visivyotambulika. Gezeti moja la Kuwait ndilo lililoripoti mkasa huo.
(ii) Watu wanakanganyikiwa na kukosa ainisho la viumbe hawa. Wanashindwa kuwaainisha viumbe hawa wasiotambulika, hasa kwa sababu kasi ya vyombo vyao ni kubwa mno kuliko ile ya vyombo walivyotengeneza binadamu.
(iii) Mimi (Prof. Ashqar) nina hakika kuwa viumbe hao wanatoka katika jamii ya Majini ambao wanaishi papa hapa duniani na ambao nimewazungumzia kwa marefu na mapana katika Kitabu changu, “The Worlds of the Jinn and the Devils”.
Katika kitabu hicho, nimeeleza uwezo wa Majini ikiwa ni pamoja na kasi ya mwendo wao inayozidi kasi ya sauti au mwanga. Vilevile wamepewa uwezo wa kujitokeza kwa maumbile mbalimbali na wana uwezo wa kuwatokea binadamu kwa maumbo tofauti.
Kwa hiyo, kwa rehema ya Mwenyezi Mungu, umetudhihirikia ukweli kuhusu viumbe hao. Tunaiona hali ya kuchanganyikiwa inayowakumba watu wasio na elimu tuliyonayo kuhusu viumbe hao. Hivyo, ni muhimu kwetu kutumia rasilimali-akili na rasilimali-fedha kufanya tafiti za kuwafaa walimwengu.
Baadhi ya watu wameuliza kwa nini viumbe hawa wasiotambulika wameonekana kujitokeza katika zama zetu wakati ambapo hawakuonekana katika zama za nyuma? Jawabu ni kwamba, Majini, katika mipango-kazi yao, hutumia chochote kinachoonekana kuwa ni kitu cha wakati uliopo. Katika zama hizi, maendeleo ya sayansi ndio mtindo wa zama hizi.
Hivyo, Majini nao huwababaisha watu kwa kutumia kitu kinachowavutia binadamu. Hivi leo watu wanatafiti uwezekano wa kuwepo viumbe katika sayari nyinginezo, kwa sababu hiyo, majini nao hujitokeza kwa umbile la vitu visivyotambulika (UFOs) ili kuwababaisha na kuwahadaa wanadamu.
Kuna wakati Majini huwatokea baadhi ya watu na kujitambulisha wazi kuwa wao ni Majini. Wakati mwingine, hujitokeza na kudanganya kuwa wao ni Malaika. Wakati mwingine huwatokea wanadamu na kujiita “misukule”.
Watu hubabaika na kusema kuwa kumbe‘fulani hajafa’ au ‘fulani kafufuka’, wakati kumbe huyo ni Jini ambaye kaja kwa umbile la ‘marehemu’. Majini wanaokuja kwa sura hii hujiita, “wao ni binadamu wasioonekana” au utasikia watu wakisema ‘vivuli’. Na wakati mwingine, Majini huwatokea watu na kudai kuwa wao ni ‘Mizimu’.
Mambo yote haya yamekuwa yakisimuliwa na watu tangia zama na zama. Wakati mwingine, Majini humsemesha mtu moja kwa moja, na wakati mwingine, husemesha watu kupitia kwa mtu kwa kutumia ulimi wake kwa muda fulani.
Hili ndilo tatizo ambalo hujitokeza hata kwa wanafunzi wanaoanguka mashuleni na kuchekacheka ovyo. Ni kwamba, maumbile yao, wakati huo, hayawawakilishi wao wenyewe, bali yanatumiwa na Majini. Hata wanaposemeshwa, sio wao wanaojibu.
Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Nkya, alijaribu kulifafanua tatizo hili kisayansi zaidi akilinasibisha na hali ambayo kwa lugha ya Kiingereza inaitwa ‘Hysteria’. Maelezo yake yalielemea zaidi katika ainisho la Kamusi ya Kiingereza.
Labda tuseme kwa Kiswahili chepesi tu kuwa, neno hilo lina maana ya hali ya kuchetuka, kurukwa na akili, kupandwa mzuka, kuwa chepe kiasi cha kupoteza uwezo wa kujitambua.
Hiyo ni hali ambayo mtu huchagizwa na jambo fulani kama kuimba au kucheza, na kadhalika. Hali hii ikizidi sana mtu huweza hata kuvua nguo hadharani. Na pia hofu inapozidi, mtu anaweza kupatwa na hali hiyo. Mathalani, mtu kapimwa damu, bila kutarajia, akakutwa na virusi vya Ukimwi, ni wazi atarukwa na akili na anaweza kusema mambo yasiyoeleweka.
Lakini kadhia ya wanafunzi ni tofauti kabisa. Na si kwamba hali hiyo huwatokea wakati wa mitihani. Haihusiani na hofu wala furaha ya wanafunzi. Ni hali tofauti sana. Hebu fikiria kitendo cha watoto kuanguka kwa pamoja, au kushindwa kutembea kwa pamoja. Hapa huwezi kulihusisha ainisho hilo la kamusi.
Wizara haiwezi kuitolea hali hii ufafanuzi tofauti na ule wa kisayansi ambao si sahihi. Hao ni Majini kama wanavyojieleza wenyewe kwa baadhi ya wanafunzi hao. Uzuri wapo hata watoto ambao hawasomi shule lakini hali hiyo huwapata.
Na ukitaka kuthibitisha kuwa hiyo ni hali tofauti, ni pale muhusika anapopigwa kipigo kikali, lakini haumii wala kujeruhiwa hata kidogo. Lakini kama angepigwa kipigo hicho kwa sababu ya hysteria, angeumia au kujeruhiwa vibaya sana! Hii si imani ya kishirikina hata kidogo. Ni imani yenye uhalisia unaothibitika kimaumbile.
Na wakati mwingine, Majini huwajibu watu kwa njia ya kuandika. Kwa kweli wana uwezo wa kufanya mengi mengineyo. Wanafahamika kwa uwezo wao wa kuwabeba watu juu-juu kwa njia ya upepo kutoka sehemu moja, na kuwapeleka sehemu nyingine. Hii inahusiana na ule uwezo wa wachawi au wawanga kuruka na ungo.